Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Mheshimiwa Farida Mgomi, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ileje kwa kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha 2025/2026, hatua aliyosema imechangia kuimarisha uwezo wa Halmashauri katika kutekeleza miradi na shughuli mbalimbali za maendeleo wilayani hapa.
Mheshimiwa Mgomi ametoa pongezi hizo wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) kilichofanyika tarehe 20 Januari 2026 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya uliopo Itumba. Katika kikao hicho, amewataka wasimamizi wa sekta ya mapato kuendelea kusimamia kwa karibu na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa ubora zaidi ili kuiwezesha Halmashauri kusonga mbele kimaendeleo.
Aidha, Mkuu wa Wilaya amezipongeza Taasisi za Serikali zilizopo wilayani Ileje kwa utendaji bora wa kazi, akibainisha kuwa jitihada zao zina mchango mkubwa katika kuimarisha ustawi wa wananchi na kufanikisha azma ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwaletea Wananchi maendeleo endelevu.
Kikao hicho cha DCC kilijadili na kupitia bajeti pamoja na mpango kazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Ambapo kilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo, wazee wa kimila na wazee maarufu, viongozi wa dini, viongozi wa chama na serikali pamoja na wawakilishi wa taasisi za serikali, ambao kwa pamoja walitoa maoni na mapendekezo ya kuimarisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo wilayani Ileje.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa