Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Mheshimiwa Farida Mgomi, leo amefanya ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara ndani ya wilaya hiyo, akilenga kukagua maendeleo ya kazi zinazoendelea katika maeneo mbalimbali.
Akiwa katika ziara hiyo, Mheshimiwa Mgomi ametembelea mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Isongole hadi Isoko, mradi unaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 74.167. Katika hatua hiyo, alifika katika kambi ya wakandarasi kujionea maandalizi ya awali kuelekea utekelezaji wa mradi huo mkubwa ambao unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 27 na nusu.
Katika muendelezo wa ziara yake, Mkuu huyo wa wilaya ametembelea pia mradi wa upanuzi wa barabara ya Ndembo–Ngana iliyopo Kata ya Ikinga. Mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 8.820, umekamilika kwa asilimia 40.1 na unatarajiwa kutekelezwa kwa muda wa miezi 12. Aidha, miradi mingine aliyotembelea ni pamoja na upanuzi wa barabara ya Sange–Lubanda pamoja na ujenzi wa daraja la Mto Sange, ambayo yote inalenga kuboresha miundombinu ya usafiri na kuimarisha uchumi wa wananchi wa Ileje.
Mheshimiwa Mgomi ametoa wito kwa TANROADS pamoja na wasimamizi wa miradi hiyo kuhakikisha wanatekeleza kazi kwa ufanisi na viwango vinavyostahili, ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi. Ameeleza kuwa miradi hiyo ina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hivyo ni lazima iharakishwe bila kuathiri ubora wake.
Kwa upande mwingine, Mkuu huyo wa Wilaya amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipatia Wilaya ya Ileje fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hasa katika sekta ya miundombinu ya barabara. Amesisitiza kuwa uwekezaji huo utaifungua Ileje kiuchumi na kuongeza fursa za maendeleo kwa wananchi, hali itakayochangia kwa kiasi kikubwa ustawi wa jamii katika wilaya hiyo.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa