Katika kahakikisha kero za wananchi zinatatuliwa na kupatiwa ufumbuzi kwa wakati Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemas Mwangela amekutana na waathirika wa upanuzi wa Barabara ya Mpemba-Isongole na kuwapa majibu kulingana na kero ya kila mmoja.
Ziara hiyo ya siku moja Wilayani Ileje,ilimwezesha kukutana na wahanga hao kutoka vijiji vya Isongole na Izuba kwenye viwanja vya Sekondari ya Ileje kisha kwenda kwenye maeneo ya wakazi hao yaliyoathirika ili kujionea hali halisi ikilinganishwa na maelezo yao.
Akiwa na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Mkoa,TANROAD Mkoa wa Songwe,Viongozi wa Wilaya ya Ileje pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM ) Mwangela alipata fursa ya kuwasikiliza wananchi hao baada ya kila mmoja kuelezwa iwapo anastahili fidia au la.
Kilio cha wengi kwa kiongozi wao kilikuwa ni kuhitaji fidia kutokana na madai yao kuwa barabara ndiyo iliyowakuta na hata kama hawatakiwi kuhama kwenye maeneo yao bado majengo yao yameathiriwa na mitambo inayojenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Tinesi Shimwela mkazi wa Kitongoji cha Mbezu katika Kijiji cha Isongole alisema kuwa ujenzi wa barabara umemsababishia kifusi kikubwa mlangoni kwake hali iliyopelekea Mkuu wa Mkoa atoe maagizo kwa Mkuu wa Wilaya kwenda kujionea jinsi hali ilivyo kwa bibi huyo.
Bi.Sevelina Kajange aliyemwakilisha Abeli Mwaweza aliomba TANROAD kutoa majibu ya wazi kwa wananchi upanuzi wa barabara unapofanyika badala ya kuchukua muda mrefu hali inayoathiri ujenzi wa nyumba kwa wananchi na kuathiri maendeleo.
Akijibu kero hizo,Mkuu wa Mkoa alisema kuwa sheria za barabara hazipo tu kwa wananchi wa hali ya chini bali hata kwa viongozi wa serikali hata matajiri kama ilivyotokea kwenye upanuzi wa barabara ya Ubungo Jijini Dar-es-Salaam.
Hata hivyo,alipofika kwenye maeneo ya waathirika hao alishuhudia tofauti kubwa ya maelezo yao na hali halisi aliyoiona huku akiwataka wananchi kutoa taarifa sahihi kinyume na hivyo inakuwa ukiukwaji wa sheria.
Siku kadha zilizopita Mkuu wa Mkoa alipofanya ziara wilayani Ileje aliweza kupokea kero toka kwa wananchi wakidai kutojua hatima yao baada ya upanuzi wa barabara hiyo hali iliyopelekea kuundwa kwa timu ya watalaam ambao ndio walitoa majibu kwa wananchi baada ya kukutana nao katika maeneo yao
Hata hivyo masaa kadhaa baada ya kiongozi huyo kuondoka Mkuu wa Wilaya ya Ileje akitekeleza maagizo aliweza kufika kwa Bibi Tinesi Shimwela na kujionea hali ya kuwepo kwa kifusi karibu na nyumba yake na akatoa maagizo kwa wahusika kukitoa ingawa hakikuwa kama alivyoeleza.
Kwa upande wa wakazi wa Izuba kulikuwa na ukweli hivyo Mkuu wa Wilaya kaliagiza timu husika kufika maeneo yale na kukutana na wahusika.
Ujenzi wa barabara hiyo ulianza takribani miaka miwili iliyopita ukiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi CCM Na Ahadi za Mhe.Rais Magufuli kwa wakazi wa Ileje ambapo katika ziara zote mbili kabla ya kuwa Rais aliweza kuahidi kutekeleza kwa vitendo ahadi hiyo.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa