Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Bi. Nuru Waziri Kindamba, amefungua rasmi semina ya mafunzo ya Mfumo wa Taarifa za Shule (SIS – School Information System) inayowahusisha Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje. Semina hiyo inalenga kuwajengea uwezo viongozi wa shule katika matumizi sahihi ya mfumo wa kidijitali wa ukusanyaji na uwasilishaji wa Taarifa za Elimu.
Akizungumza katika hotuba ya ufunguzi wa Semina hiyo, Bi. Kindamba amewataka Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu kujifunza kwa umakini matumizi ya mfumo wa SIS ili waweze kujaza na kutoa taarifa pamoja na takwimu sahihi. Amesisitiza kuwa usahihi wa taarifa katika mfumo huo ni msingi wa kupata manufaa lengwa katika kupanga na kuboresha huduma za Elimu ngazi ya Halmashauri na Taifa kwa ujumla.
Aidha, Bi. Kindamba amewahimiza Walimu kuzingatia uwajibikaji kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuleta matokeo mazuri ya kitaaluma kwa wanafunzi, hususan waliopo katika madarasa ya mitihani ambao ni Darasa la Saba, Kidato cha Nne na Kidato cha Sita. Vilevile, ametoa rai kwa walimu kushirikiana, kufanya kazi kwa uwazi na kudumisha mshikamano ili kupunguza na kuondoa migogoro pamoja na changamoto za kitaaluma shuleni.
Semina hiyo ya mafunzo itafanyika kwa siku mbili, ikilenga kutoa elimu kwa Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu kuhusu namna ya kujaza taarifa sahihi katika mfumo wa SIS. Taarifa hizo ni pamoja na Taarifa za Kitaaluma, Idadi Ya Wanafunzi, Idadi Ya Walimu, Thamani ya Rasilimali zilizopo shuleni, Miundombinu ya Shule pamoja na Huduma Mbalimbali Zitolewazo Shuleni Kwa Njia Ya Kidijitali. Mfumo huo unalenga kupunguza uingizaji wa Taarifa kwa kurudia mara kwa mara kutokana na awali kukosekana kwa mfumo madhubuti wa utoaji wa Taarifa.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa