Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa Songwe Mhe.Waziri Kindamba alipokuwa akizindua Kampeni ya Polio hapo Novemba, 30, 2022 katika Hospitali ya Vwawa huku watoto 342,692 wakitarajiwa kupata chanjo hiyo.
Mhe.Kindamba ametoa wito kwa wazazi na walezi wote mkoani humo kupeleka watoto wenye umri chini ya miaka mitano katika vituo vya kutolea huduma za afya ili wapate chanjo ya matone ya Polio au kutoa ushirikiano kwa watalaam wa afya watakaopita nyumba kwa nyumba kuwapatia chanjo watoto hao.
“Ugonjwa wa polio umeripotiwa katika nchi jirani za Malawi na Msumbiji,hivyo sisi tukiwa majirani ni lazima tuchukue tahadhari kwa kuwakinga watoto wetu kwa chanjo kabla ugonjwa huu haujaingia hapa nchini,kwani kinga ni bora kuliko tiba”Alihimiza Mhe.Kindamba.
Kiongozi huyo aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt.Samia Suluhu Hassan itahakikisha kuwa inawalinda watoto kwa gharama yoyote akisema kuwa hawa ndio Taifa la Tanzania ya kesho.
Bi.Happiness Seneda katibu Tawala wa Mkoa huo amesema kuwa watalaam wa afya wamejipanga vya kutosha kuhakikisha wanawafikia watoto wote walengwa kwa zaidi ya asilimia 100% kama walivyofanya katika awamu zilizopita.
Alibainisha kuwa awamu ya kwanza iliyofanyika Machi ilikuwa asilimia 117, Awamu ya Pili Mei 128 % na Awamu ya Septemba walifikia watoto kwa asilimia 119%.
Moses Lyimo Mratibu wa chanjo ya polio mkoani humo alisema kuwa Kampeni ya Awamu ya Nne wanatarajia kuwafikia watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano hata kama mtoto atakuwa amepata chanjo siku moja kabla ya uzinduzi anatakiwa kupata kwani ziada haina madhara yoyote.
Ikumbukwe kuwa mkoa wa Songwe una jumla ya wilaya nne ambazo ni Ileje,Mbozi,Momba na Songwe huku ukiwa na halmashauri tano ambazo ni Ileje,Mbozi,Momba Songwe na Mji wa Tunduma.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa