DED Ileje awapo Somo Maafisa Ugani,awataka waache kukaa ofisini na kwenda vijijini kuhudumia wananchi
Wakati shughuli za uvunaji wa nafaka zikiwa zimepamba moto Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje mkoani Songwe amewataka Mafisa Ugani kwenda kwa wakulima na wafugaji ili kusimamamia kwa karibu sekta hiyo.
Mkurugenzi huyo Ndugu Haji Mnasi ameyasema hayo wakati wa kikao kazi cha siku moja cha wataalam hao kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo kikilenga kujadili masuala mbalimbali ya kilimo na mifugo.
‘’Utendaji kazi wenu lazima ulete matokeo chanya kwa wananchi yatakayobadili hali duni za maisha na kwenda kwenye hali bora zaidi mkiwa wabunifu kulingana na maeneo yenu ya kazi’’alisisitiza kiongozi huyo.
Alisema kuwa,huu si wakati wa kukaa ofisini kama ilivyokuwa imezoeleka bali ni wakati ambao wataalam wanatakiwa kwenda kwa wananchi ili kubadali njia za uzalishaji mali zilizopitwa na wakati na kuwawezesha kutumia teknojia ya kisasa.
Akizungumza katika kikao hicho,Afisa Kilimo na Umwagiliaji wa Halmashauri hiyo Ndugu Herman Njeje aliwataka wataalam hao kuwa kioo katika jamii kwa jinsi wanavyoendesha shughuli zao binafsi za kilimo ili wananchi waweze kuiga kwa vitendo badala ya kuendelea kutoa nadharia.
‘’Fanyeni shughuli zenu kitaalam kwani jamii ina imani kubwa sana na idara hii kwa vile inagusa moja kwa moja maisha yao ya kila siku,hivyo mafanikio yao yanategemea sana taaluma juhudi zenu”alisema Ndugu Njeje.
Wakizungumza katika kikao hicho, Maafisa Ugani hao waliomba mawasiliano ya mara kwa mara yafanyike ili waweze kuwajulisha wananchi juu ya mabadiliko yanayotokea pamoja na taarifa muhimu toka ngazi za juu kuwafikia wananchi ili kutopata taarifa zilizopitwa na wakati.
Tayari Halmashauri hiyo ilishatekeleza agizo la serikali la kupunguza Maafisa wa Idara hiyo katika Ofisi ya Mkurugenzi ambapo kati ya nane waliokuwepo tayari watano walishapangiwa vijijini huku wakibaki maafisa watatu,lengo la serikali likiwa ni kusogeza huduma kwa wananchi.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa