Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) kwa mwaka 2025 Mkoani Songwe yameadhimishwa katika Wilaya ya Mbozi. Katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Mheshimiwa Farida Mgomi amemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mheshimiwa Daniel Chongolo Kama mgeni rasmi katika maadhimisho ya sherehe hizo.
Akihutubia wafanyakazi waliokusanyika katika viwanja vya Maadhimisho, Mheshimiwa Mgomi amewasihi Wafanyakazi kushiriki kwa ukamilifu katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Mwezi Oktoba mwaka huu, kwa lengo la kuchagua Viongozi bora watakaosimamia masilahi ya wafanyakazi na ustawi wa Taifa kwa ujumla.
Aidha, alibainisha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuboresha na kusimamia vyema ustawi na masilahi bora ya wafanyakazi nchini. Alieleza kuwa hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa ajira mpya, kuboresha mazingira ya kazi, kulipa madeni na malimbikizo ya watumishi wa umma.
Katika kuimarisha Nidhamu ya Matumizi ya Rasilimali, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya aliwataka Waajiri wote kuacha kuzalisha madeni mapya yasiyokuwa na msingi, ambayo yamekuwa mzigo kwa serikali. Alisisitiza kuwa ni muhimu kuhakikisha kila haki ya mfanyakazi inalindwa kwa mujibu wa Sheria ili kuimarisha uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi. Pia, alizitaka Halmashauri zote ndani ya Mkoa wa Songwe kufanya marekebisho ya Mishahara kwa haraka pindi mtumishi anapopanda daraja. Alieleza kuwa hakuna sababu ya msingi ya kuchelewesha mchakato huo, kwani ucheleweshaji huo unachangia kuibua madeni yasiyo ya lazima ambayo yanaongeza mzigo kwa Serikali.
Akihitimisha hotuba yake, Dc Mgomi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, aliwataka Waajiri wote kuendelea kuzingatia misingi ya Haki, Sheria na Kanuni katika kushughulikia masuala yanayohusu masilahi ya Watumishi. Maadhimisho haya yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Kisiasa na wa Vyama vya Wafanyakazi, yakiwa yamepambwa na maandamano ya amani, burudani kutoka kwa vikundi vya sanaa, na maonyesho ya shughuli za wafanyakazi kutoka Sekta mbalimbali.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa