Maadhimisho ya Siku ya Mazingira yafanyika Ileje,dc azitaka shule zote kuunda Klabu za Mazingira
Wilaya ya Ileje imeungana na Dunia nzima kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani huku Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe.Farida Mgomi akizitaka shule za msingi na sekondari kuunda Klabu za Mazingira.
Ameyatoa maagizo hayo katika Kijiji cha Chitete kwenye viunga vya Shule ya Msingi Chitete palipofanyika maadhimisho hayo kiwilaya.
Mhe. Mgomi alisema kuwa watoto wakijengewa uwezo katika umri huo wanaweza kuwa chachu katikati uhifadhi wa mazingira kiwilaya,kitataifa hadi kidunia.
Alitoa kauli hiyo kufuatia shule tatu tu ambazo ni Sekondari ya Msomba,shule za msingi Bulanga na Namaselele zilizopo kata ya Malangali kuwa ndizo zenye klabu za mazingira zikiwa zimeundwa na halmashauri kwa kushirikiana na Kamisheni ya Bonde la Mto Songwe.
Taarifa ya halmashauri kwa Mgeni Rasmi ilieleza kuwa jumla ya miti 2716 rafiki wa mazingira imepandwa kwenye vyanzo vya maji vya Itumba,Iyela pamoja na Ilumba,huku Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wakigawa kwa wananchi miche 16850 ya miti ya aina mbalimbali.
Wilaya ya Ileje hususani Tarafa ya Bundali imejitahidi sana kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti huku wenzao wa Tarafa ya Bulambya ambayo ipo ukanda wa chini unaopata mvua kidogo wakiendelea kusuasua.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa