Kamati ya Fedha, Uchumi na Mipango (FUM) ya Halmashauri ya Wilaya ya Ileje imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika wilaya hiyo. Ziara hiyo ililenga kutathmini hatua za utekelezaji wa miradi yenye lengo la kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi, hususan katika sekta za afya, elimu, mazingira na utawala.
Katika tarafa ya Bulambya, kamati hiyo ilikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika hospitali ya wilaya – Itumba, ambapo halmashauri imepokea shilingi milioni 350 kwa ajili ya kukamilisha mradi huo ambao umefikia asilimia 80 ya utekelezaji. Pia walikagua jengo la utawala la halmashauri ambalo limegharimu kiasi cha shilingi bilioni 2, pamoja na mradi mkubwa wa upanuzi wa shule ya sekondari Izuba kwa ajili ya kuanzisha kidato cha tano na sita, ambao unajumuisha madarasa manne, nyumba moja ya watumishi (2-in-1), mabweni mawili, na vyoo, kwa gharama ya shilingi milioni 480.
Miradi mingine iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa bweni katika shule ya sekondari ya wasichana Ileje unaogharimu shilingi milioni 130 na ambao umefikia asilimia 30 ya utekelezaji, pamoja na mradi wa usafi na mazingira katika zahanati ya Ikumbilo unaohusisha ujenzi wa kichomea taka, mashimo ya majivu na kondo la nyuma kwa akina mama waliojifungua, pamoja na sehemu ya kunawia mikono, kwa gharama ya shilingi milioni 16.5.
Kamati ya FUM imetoa pongezi kwa wasimamizi wa miradi hiyo kwa usimamizi thabiti na utekelezaji mzuri wa miradi, huku ikisisitiza umuhimu wa kukamilisha miradi hiyo kwa wakati ili ianze kutoa huduma stahiki kwa wananchi. Vilevile, kamati hiyo imemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuipatia wilaya hiyo fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hatua inayochochea ustawi na maendeleo ya wananchi wa Ileje.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa