Na:Daniel Mwambene,Ngulilo-Ileje
Jeshi la Akiba(mgambo) wilayani Ileje mkoa wa Songwe limetakiwa kuwafichua wakwamishaji wa maendeleo ili kuonesha uzalendo kwaTaifa.
Wito huo ulitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ileje ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mhe. Joseph Mkude alipokuwa akifunga mafunzo yaliyochukua zaidi ya miezi mitano kwa jeshi hilo katika Kata ya Ngulilo.
Alisema kuwa vipo vitendo kadha vya kiharifu vinavyofanywa katika jamii na kutoripotiwa kwenye mamlaka zinazohusika.
Mhe. Mkude alibainisha vitendo hivyo visivyokubalika kuwa ni kwa baadhi ya watu wakiwemo watumishi wa umma kunywa pombe muda usiokubalika kisheria,utoaji na upokeaji rushwa pamoja na kuendekeza migogoro ya ardhi ambayo ni mikubwa kwa kata hiyo na wilaya nzima kwa ujumla hususani katika Tarafa ya Bundali ambako ardhi ina thamani kubwa.
"Mnapoyaona haya msikae kimya,kwani madhara yake si kwenu tu bali hata kwa vizazi vijavyo kuweni mfano wa kuyachukia na kuyaripoti bila woga"alisisitiza Mhe.Mkude.
Akitolea mfano wa Miradi ya Maendeleo inayojengwa katika wilaya nzima ya Ileje ni jukumu la jeshi hilo kutoa taarifa kwake na kwa viongozi wengine pale wanapoona dalili za uchakachuaji badala ya kusubiri mambo kuharibika.
Aidha kiongozi huyo alilaani kwa baadhi ya walengwa kushindwa kufikia mwisho wa mafunzo ya mafunzo akisema huo umekuwa ni mzigo wa wilaya na Taifa kwa ujumla kwa kuwa wamekosa stadi muhimu za maisha.
Wahitimu hao wapatao 114 kati ya 293 waliokuwa wameandikishwa waliwaomba viongozi wa Kata ya Ngulilo kutokuwa chanzo cha ukwamishaji wa mipango ya serikali.
Akisoma risala yao kwa Mgeni Rasmi wakati wa kufunga mafunzo hayo Imma Asajenie alisema kuwa kuacha mafunzo kwa vijana waliokuwa wameandikishwa kulichangiwa kwa kiasi fulani na viongozi wa kata hiyo kwa kushindwa kuwachukulia hatua.
Wakati wa mafunzo haya vijana hawa walishiriki katika shughuli za maendeleo kwenye kata yao kwa kulima barabara,kufyatua matofali pamoja na kukusanya mawe kwaajili ya ujenzi wa daraja la kuelekea kijiji cha Shiringa.
Ikumbukwe kuwa kila mwaka mafunzo kama haya hufanyika kwa kata moja ambapo mwaka 2016 yalifanyika katika Kata ya Ibaba,2017 Ngulilo na 2018 yataiangukia kata nyingine.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa