Jeshi la Akiba(mgambo) lafundwa kuhusu uzalendo
“Uzalendo,uzalendo” ni maneno yaliyotawala kwenye ufunguzi wa Mafunzo ya Jeshi la Akiba (mgambo) wilayani Ileje huku watumishi wa serikali wakijitosa,yumo pia mkimbiza Mwenge wa Uhuru mara mbili kitaifa.
Hatimaye mafunzo kwa Jeshi la Akiba lililokuwa likijulikana kama mgambo yameanza katika Kata ya Itumba ambayo ni Makao Makuu ya Wilaya hiyo,viongozi wakiwataka walengwa kutanguliza uzalendo mbele.
Akizungumza na askari tarajali hao Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya ambaye ni Mkuu wa Wilaya hiyo Ndugu Joseph Mkude alisema kuwa wanafunzi hao hawana budi kuwa vioo vya jamii katika kupinga na kuzuia vitendo vya uharifu vinavyofanyika.
“Idadi ya askari waliopo hawatoshi ndiyo maana serikali yetu ilibuni jeshi hili la akiba ili liweze kuziba mapengo haya badala ya kutegemea Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na vyombo vingine vya ulinzi katika kulinda usalama wa nchi yetu”alisistiza kiongozi huyo.
Aliwataka kutofumbia macho viashiria vyovyote vinavyoonesha dalili ya kukwamisha kasi ya utendaji wa serikali ya awamu hii ya tano akiwataka kuipiga jeki halmashauri yao katika kuongeza makusanyo ya mapato.
Mhe.Mkude aliwapongeza askari hao kwa ushiriki wao katika masuala ya usafi wa mazingira pamoja na mazoezi akitaka wananchi kuwaunga mkono uzalendo huo wa kuacha shughuli zao na kutekeleza mtaala wa mafunzo hayo.
Naye Kanali Zonobius Kapinga ambaye ni Mshauri wa Jeshi hilo mkoani Songwe aliyewatembelea askari hao aliwataka kutotanguliza maslahi yao binafsi badala yake waweke utaifa mbele akisema ndiyo ishara ya uzalendo.
“Mnapohitajika kufanya kazi kamwe msiulize mtalipwa shilingi ngapi,kwani tunawaanda kuwa walinzi wa taifa letu mkiwa sehemu ya JWTZ sitaraji mtakuwa chanzo cha kuvunja sheria za nchi yetu na kwenda kutupwa magerezani”aliwaambia.
Alisema kuwa,mwisho wa mafunzo hayo ni matarajio ya jeshi kuwa wataacha alama ya kitu walichofanya kwa vitendo kama ambavyo baadhi ya watu wameshaacha alama zao katika jamii.
Awali,akisoma taarifa kwa mgeni rasmi mmoja wa wakufunzi afande Isaya Muyoba alisema kuwa kumekuwa na mwitikio mkubwa wa mafunzo hayo ambapo awali walianza wanafunzi zaidi ya 20 na kufikia zaidi ya zaidi hadi sasa.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa kwa mara ya kwanza tofauti na miaka iliyotangulia mafunzo hayo yanashirikisha pia baadhi ya watumishi wa umma ambao waliitikia wito wa Mkuu wa Wilaya aliyewataka walikuwa tayari kujiunga na mafunzo hayo kufanya hivyo.
Akizungumza na mwandishi wetu mmoja wa watumishi hao wa serikali Ndugu Wito Mlemelwa ambaye aliwahi kimbiza Mwenge wa Uhuru mara mbili kitaifa 2012 na 2014 alisema kuwa yeye kama mtanzania na mzalemdo hana budi kushiriki vema fursa kama hizo zinapojitokeza.
Alisema kuwa anaamini kuwa alipokuwa anajiunga na mafunzo hayo ni dhahili atakapokuwa anamaliza atatoka na vitu vipya ambavyo vitamsaidia yeye na jamii inayomzunguka.
Mafunzo hayo yamekuwa yakifanyika kwa kata moja kwa kila mwaka katika kila wilaya ambapo kwa wilaya ya Ileje mwaka juzi yalifanyika katika Kata ya Ibaba na mwaka uliopita yalifanyika katika Kata ya Ngulilo ambapo Mkuu wa Wilaya alikemea baadhi ya viongozi wa kisiasa kuwa kikwazo kwa maslahi binafsi.
Ikumbukwe kuwa,maeneo mengi yas vijijini jeshi hili limekuwa likifanya vizuri katika masuala ya ulinzi na kwa wale wahenga wanakumbuka jinsi lilivyoshiriki kumng’oa Idd Amin alipovamia kule Kagera na kasha kumfurumisha hadi nje ya Uganda.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa