Jumla ya watoto 15 wa Shule za Msingi na Sekondari waliokuwa wameachishwa shule wamerejeshwa shuleni na kuendelea na masomo tangu mwezi Januari hadi mwezi huu Novemba mwaka huu.
Taarifa ilitolewa na Afisa Ustawi wa Jamii Bi.Tabitha Swila kwenye kikao cha siku moja cha Kamati ya Kutokomeza vitendo vya Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo kikijumuisha Ofisi ya Mkuu wa Wilaya,Baadhi ya Wataalamu toka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji pamoja na viongozi wa dini.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa pia wilaya hiyo imefanikiwa kuwaondoa watoto watatu chini ya miaka mitano waliokuwa waliokuwa katika mazingira hatarishi na kuwapeleka katika kituo cha kulelea watoto wa aina hiyo kilichopo katika Hospitali ya Misheni ya Mbozi.
Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho wamewataka wanaume pia kutokaa kimya pale wanapofanyiwa vitendo vya ukatili na wanawake kwani kwa kufanya hivyo huweza kuhatarisha afya zao ikiwemo kujiondoa uhai kwa kujinyonga.
Aidha wametoa angalizo kwa wanafunzi kujiepusha na mapenzi hali inayochangia kuzalisha watoto wa mitaani hivyo kuongeza vitendo vya unynyasji na ukosaji wa matunzo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo Katibu Tawala Ndugu Matias Mizengo alisema kuwa zaidi ya watoto 220 wamefanyiwa vitendo vya ukatili mkoani Songwe huku zaidi ya watoto 40 wakifanyiwa vitendo hivyo wilayani Ileje.
Akifunga kikao mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Ndugu Haji Mnasi ameitaka jamii kuungana katika mapambano dhidi ya ukatili wa wanawake na watoto.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa