Katika hatua isiyotarajiwa Mkuu wa Wilaya ya Ileje Ndg.Joseph Mkude amewasamehe wote walioiba miche ya miti iliyotarajiwa kupandwa kwenye barabara ya lami inayoendelea kujengwa akisema sasa somo la upandaji miti limeeleweka.
Aliyasema hayo mara baada ya kukamilisha zoezi la upandaji miti lililoongozwa na yeye kando kando ya Barabara ya Mpemba hadi Isongole zaidi ya Km 50.
“Jana nilitaarifiwa kuwa miche ya miti iliyokuwa imewekwa nje ya Ofisi ya kijiji cha Isongole imeibwa na wananchi,kwa kweli nawapongeza waliofanya hivyo huo ni wizi mtakatifu maana yake somo limeeleweka kwa wananchi wangu”alisisitiza kiongozi huyo.
Alipotoa kauli hiyo,ambayo haikutarajiwa na wengi alipigiwa makofi na wananchi huku wakishangilia kuashiria kupata msamaha hasa kwa viongozi wa serikali ya kijiji ambao walikuwa wakihofia kuadhibiwa kwa uzembe.
DC Mkude alimwagiza Mkurugenzi kuhakikisha halmashauri ya wilaya na taasisi zake zinaanzisha vitalu vya miti ili kwa msimu ujao iweze kugawa kwa wananchi ambao wameonesha kuhitaji kwa kiasi kikubwa.
Ukweli wa kauli hiyo uliweza kuungwa mkono kwa vitendo pale wakati wa mgao wa miche hiyo kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari walivyokuwa waking’ang’aniana ili angalau kupata miche hiyo.
Katika zoezi hilo zaidi ya miche 4000 iliyotolewa na Wakala wa Misitu hapa nchini TFS iliweza kupandwa huku mingine wakipewa wananchi.
Lengo za upandaji wa miti katika barabara hiyo kwa mujibu wa Mhe.Mkude ni kushirikisha jamii nzima kuifanya Tanzania kuwa ya kijani ukiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika kutunza mazingira.
Pia zoezi hilo ambalo ni endelevu hadi mpakani mwa Wilaya hiyo na Wilaya ya Momba katika Kijiji cha Nandanga na maeneo yote ya wilaya hiyo ni utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan alilolitoa miaka michache iliyopita juu ya umuhimu wa upandaji miti.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa