Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Mheshimiwa Farida Mgomi,ametoa pongezi kwa wasimamizi wa Miradi ya ujenzi wa miundombinu ya Shule ikiwemo vyoo, vitakasa mikono Pamoja na mifumo ya maji kupitia fedha za SWASH
Mheshimiwa Mgomi ametoa pongezi hizo mara baada ya kufanya ziara na kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo katika Shule ya Msingi Ishenta iliyopo katika katika Kata ya Ndola pamoja na Shule za Msingi Itumba na Nyerere zilizopo katika Kata ya Itumba wilayani hapa.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Mgomi amemshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Daktari Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za kuboresha na kujenga miundombinu mipya katika shule zilizopo wilayani hapa.
Aidha, Mheshimiwa Mgomi ameisifu miradi hiyo kwani itasaidia wanafunzi kuepuka magonjwa ya mlipuko kama kuhara na kutapika , sambamba na kuimarisha afya na taaluma za wanafunzi kutokana na uwepo wa miundombinu ya vyoo bora pamoja na maji safi ya kunawa mikono mara baada ya kutoka chooni.
Sambamba na hayo Mkuu wa wilaya ametoa rai kwa wasimamizi wa miradi hiyo kumalizia sehemu chache zilizobaki ili miradi ianze kutoa huduma kwa wanafunzi. Miradi hiyo ya SWASH imefikia asilimia 98 ili ianze kutoa huduma.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa