Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Mheshimiwa Farida Mgomi, amewaasa wananchi wa wilaya ya Ileje kuhakikisha wanaendelea kuimarisha amani na utulivu kwa kuwakemea vikali wachochezi na wavunjifu wa amani, pamoja na kutokuwavumilia wale wanaobeza jitihada na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan zinazolenga kuimarisha na kuinua Maendeleo na Ustawi wa wananchi.
DC Mgomi alitoa wito huo wakati wa maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanzania, yaliyoadhimishwa Kiwilaya katika Kata ya Isongole, wilayani hapa. Ambapo amewahutubia wananchi waliojitokeza kusherehekea maadhimisho hayo, huku akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo endelevu, hivyo kila Mwananchi ana wajibu wa kuilinda kwa nguvu zote.
“tuendelee kuilinda amani ambayo tumeirithi kutoka kwa waasisi wa Muungano na pia Serikali ya Awamu ya Sita haipo tayari na haitowafumbia macho wale wenye nia ovu ya kubeza na kuhatarisha amani na utulivu Tunu zilizoachwa na waasisi wa Muungano huu” alisisitiza Dc Mgomi.
Mheshimiwa Mgomi aliwahimiza wananchi wa Ileje kuwa mstari wa mbele katika kushiriki shughuli za maendeleo, kuheshimu sheria na taratibu, pamoja na kudumisha mshikamano na upendo miongoni mwao kama sehemu ya kuenzi Muungano wa Tanzania.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa