Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani Ileje kimepongeza utendaji kazi unaoneshwa na watendaji wa umma kwa jinsi wanavyosimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali pamoja na maagizo ya serikali.
Pongezi hizo zilitolewa hivi karibuni na Katibu wa chama hicho wilayani humo Ndg.Albert Sitima wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo kilichofanyika hivi karibuni.
“Nawapongezeni kweli kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ambao ndio mkataba wetu na wananchi katika maeneo mbalimbali ya wilaya yetu ambayo itatupunguzia kazi kuwaelezea wananchi nini tumefanya kwa miaka mitano’’ alisema kiongozi huyo.
Katibu huyo aliongezakuwa CCM imekuwa ikiwafuatilia namna watumishi wa umma wavyosimamia miradi ya maendeleo ambayo kukamilika kwake kunawapunguzia kero wananchi ambao Mhe.Rais Magufuli amekuwa akiaagiza wahudumiwe ipasavyo.
Aliongeza kuwa Kamati ya Usalama imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha maagizo na miongozo ya serikali inafuata ili kukwendana na kasi ya Awamu ya Tano.
Pongezi hizo zinakwenda sanjari na zile zinazotolewa na viongozi wengine akiwemo Waziri wa TAMISEMI Mhe.Seleman Jafo aliyepongeza ubora wa majengo ya Hospitali ya Wilaya hiyo wakati wa ziara yake siku miezi michache iliyopita huku Mkuu wa Mkoa huyo Brigedia Jenerali Mstaafu Nicodemas Mwangela akizitaka Halmashauri zingine kuiga viwango vya ujenzi tika Ileje.
Akizungumza katika kikao hicho DC wa Wilaya hiyo Ndg.Joseph Mkude aliwataka Wahe.Madiwani kuendelea kuchapa kazi badala ya kuanza kuingiwa na hofu ya uchaguzi akiongeza kuwa matendo mazuri kwa kipindi chao yatawabeba kwenye Uchaguzi
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa