Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la Ileje, Bi. Nuru Waziri Kindamba, amefungua rasmi semina ya Mafunzo kwa Waandishi Wasaidizi na waendesha Vifaa vya Bayometriki (BVR) kwa ajili ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, awamu ya pili. Katika hotuba yake ya ufunguzi, Bi. Kindamba aliwasisitiza washiriki hao kuzingatia uadilifu, weledi na kutunza vifaa vya kazi ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia maelekezo ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Bi. Kindamba alieleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwaandaa watendaji hao kutekeleza majukumu yao kwa umahiri, ikiwemo kutumia vifaa vya bayometriki kwa usahihi na kuwahudumia wananchi kwa heshima na ufanisi. Alisisitiza kuwa vifaa vya BVR vimenunuliwa kwa gharama kubwa, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuvihifadhi na kuvitumia kwa uangalifu ili kuepuka hasara kwa serikali.
Mafunzo haya ni sehemu ya maandalizi ya awamu ya pili ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ambapo waandishi wasaidizi na waendesha vifaa vya BVR wanapewa elimu ya kina kuhusu majukumu yao, matumizi sahihi ya vifaa vya uandikishaji na umuhimu wa kutoa huduma bora kwa wananchi.
Bi. Kindamba alihitimisha kwa kuwataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa mabalozi wa uadilifu na weledi katika jamii, kuhakikisha kuwa kila mwananchi mwenye sifa anapata fursa ya kujiandikisha na kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa