“Acheni kuwaibia wakandarasi”,Waziri Kwandika
Waziri awataka watanzania walio kwenye maeneo ya miradi kuwa waaminifu,asema wizi wa mafuta unaligharimu taifa letu fedha nyingi.
Tahadhari hiyo,ilitolewa hapo jana na Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhe.Elius Kwandika alipokuwa akizungumza na wananchi kwenye kambi la Kampuni ya Kachina inayojenga barabra ya Mpemba –Momba hadi Isongole-Ileje kwa kiwango cha lami.
“Kuwaibia wakandarasi hakukwamishi tu kasi ya ujenzi wa miradi kwa wakandarasi bali hutucheleweshea maendeleo na mnapofanya hivyo mnajiibia ninyi wenyewe”alisema kiongozi huyo.
Alitolea mfano wa huko mkoani Kigoma kuwa mkandarasi aliibiwa zaidi ya lita 1200 za mafuta hali inayopunguza imani ya wakandarasi kwa wafanyakazi wao na watanzania kwa ujumla.
Aliongeza kuwa,malipo yanayotolewa kwa mafuta yaliyoibwa kwenye maeneo ya ujenzi wa miradi gharama za malipo ya bili zake hubebwa na serikali ambayo inakuwa imelipa kwenye kazi hewa.
Akitoa taarifa fupi ya hali ya mtandao wa barabara wilayani humo Mkuu wa Wilaya ya Ileje Ndugu Joseph Mkude alimwomba waziri huyo kupiga jicho kwenye barabara inayounganisha Ileje na Mbozi kupitia Vijiji vya Namwangwa na Ilanga ambapo daraja la Mto Isenga kingo zake ziliharibiwa na mvua za masika hapo mwaka jana na kuharibu mawasiliano.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe.Ubatizo Songa alimwomba waziri kuendelea kutupia macho barabara ya kutoka Ileje kwenda Kyela akisema ina umuhimu mkubwa kiuchumi na kiulinzi kwa kuwa inakwenda sanjali na mpaka wa nchi jirani.
Kwa muda mrefu kilio cha ujenzi wa barabara ya Mpemba –Isongole kwa kiwango cha lami kilikuwa kikiwafikia viongozi wa ngazi mbalimbali ambapo hata Mhe.Rais akiwa Waziri wa Ujenzi miezi michache kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 na serikali yake imekifanyia kazi na kukituliza kwa vitendo.
Wakazi wa Ileje na nchi jirani ya Malawi wana matarajio makubwa juu ya fursa zitakazofunguka mara ujenzi huu utakapokamlika.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa