Na:Daniel Mwambene, Ileje DC
RC wa Songwe ametaka wakazi wa mpakani kuishi kwa amani na nchi jirani na kutatua matatizo yanayojitokeza kwa njia ya mazungumzo.
Zikiwa ni siku chache zimepita tangu Mhe.Rais Magufuli alipotembelee nchi ya Malawi Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Mstaafu Nicodemas Mwangela amewataka wakazi wa mkoa huo kulinda na kudumisha amani na nchi jirani.
Alitoa kauli hiyo alipokuwa kizungumza wilayani Ileje na Wahe.madiwani pamoja na watendaji wa serikali kwenye ukumbi wa Hospitali ya wilaya hiyo kufuatia taarifa ya kuhamahama kwa Mto Songwe ambao ni mpaka wa Tanzania na Malawi katika Kata ya Chitete.
Kiongozi huyo ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo akifafanua baada ya Mhe.Diwani wa Chitete Joseph Kayuni kutoa taarifa ya kuhama kwa mto huo alisema wananchi wa maeneo ya mpakani hawana budi kuvumiliana katika kipindi kama hicho.
‘’Hakikisheni mnamaliza matatizo haya kwa kukaa mezani kwani sisi sote ni ndugu hili liko wazi kwa mipaka mingi halikwepeki iwe Kenya na Uganda au mataifa yoyote ile watu wa pande mbili za mataifa huwa na mahusiano makubwa ya kihistoria’’.alisisitiza kiongozi huyo.
RC Mwangela alitumia nafasi hiyo kumwagiza Mkuu wa Wilaya ya Ileje Ndugu Joseph Mkude kuhakikisha anakutanana na Mkuu wa Wilaya ya Chitipa Malawi kuhakikisha wanakaa pamoja kushughulikia tatizo hilo.
Sehemu kubwa ya mpaka kati ya Tanzania na Malawi ni Mto Songwe ambao umekuwa ukihamahama mara kwa mara na kupelekea mataifa haya mawili kuwa na mradi wa pamoja wa Bonde la Mto Songwe ambao ulizinduliwa hivi karibuni wilayani Kyela nchini Tanzania.
Wakati maagizo hayo yakitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe,tayari Wilaya ya Ileje imekuwa ikifanya vikao vya kidiplomasia na Wilaya ya Chitipa-Malawi vikilenga kuufanya mpaka huo kuwa makazi salama kwa wananchi wa pande zote.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa